Fungwa Kilozo Fungwa Kilozo Author
Title: KUHUSU MJI WA LINDI
Author: Fungwa Kilozo
Rating 5 of 5 Des:
1.0 HISTORIA YA MJI WA LINDI Mji wa Lindi ni mmojawapo ya Miji mikongwe nchini k...
1.0 HISTORIA YA MJI WA LINDI
Mji wa Lindi ni mmojawapo ya Miji mikongwe nchini kwani ulianzishwa na wafanyabiashara wa kiarabu katika karne ya 11. Baadaye wakati wa ukoloni wa Kiingereza, wafanyabiashara Wahindi walihamia na kuweka makazi katika Mji wa Lindi.
Mji wa Lindi ulikuwa makao mkuu ya Jimbo la Kusini hadi mwaka 1952 wakati makao makuu yalipohamia Mtwara kutokana na sababu za kiuchumi na mazingira mazuri ya bandari ya Mtwara. Mabadiliko hayo yalisababisha Mji wa Lindi kudumaa licha ya kuwa makao makuu ya Mkoa wa Lindi kuanzia mwaka 1971.

Halmashauri ya Mji wa Lindi ilianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1953.
1.1 UTAWALA
Kiutawala Halmashauri ya Mji wa Lindi imegawanyika katika Tarafa 1, Kata 13 na Mitaa 63. Kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002, Halmashauri ilikuwa na jumla ya watu 41,549 wakiwepo wanaume 20,300 na wanawake 21,249. Ongezeko la watu ni asilimia 1.4 hivyo inakadiriwa kuwa mwishoni mwa mwaka 2007 Halmashauri ya Mji itakuwa na watu 44,540. Wingi wa watu hao kwa kilometa moja ya mraba ni watu 141.

1.2 ENEO LA KIJIOGRAFIA
Halmashauri ya Mji wa Lindi inapatikana katika latitude 9045’ na 10045’ kusini ya Ikweta na longitude 39050 na 39036” mashariki ya Greenwichi na inazungukwa na Halmashauri ya Wilaya ya Lindi pande zote isipokuwa upande wa mashariki ambako kuna bahari ya Hindi. Ina ukubwa wa kilometa za mraba 315.
1.3 HALI YA HEWA
Halmashauri ya Mji wa Lindi ni ya joto linalofikia kati ya nyuzi joto 24C0 na 27C0. Halmashauri hii inapata mvua za wastani wa kuanzia mm 800 mpaka mm 1000 kwa mwaka. Mvua za kawaida zinaanza mwezi Novemba mpaka Januari na mvua kubwa zinaanza mwezi Machi hadi Juni.
1.4 SHUGHULI ZA KIUCHUMI ZILIZOPO
Shughuli kubwa za wakazi wa Lindi Mjini ni kama zilivyoorodheshwa hapa chini:
1.4.1 KILIMO NA MIFUGO
Kilimo ni shughuli ya uchumi inayoshirikisha watu wengi katika Halmashauri Mji wa Lindi. Asilimia 50 ya wakazi wa Halmashauri ya Mji wa Lindi ni wakulima. Shughuli ya Kilimo hufanyika katika Vijiji vya Kineng’ene, Mitwero, Tulieni na Kitumbikwela. Mazao makuu ya chakula ni muhogo, mahindi, mtama na mazao makuu ya biashara ni korosho, ufuta na nazi. Ufugaji ni shughuli inayofanywa kwa kiwango cha chini sana.
1.4.2 UVUVI
Uvuvi ni moja ya shughuli ambazo wakazi wengi wa Lindi hasa waishio kando kando ya bahari ya Hindi wanategemea ingawa zana zinazotumika kwa uvuvi ni duni, kiasi kinachofanya uzalishaji wa samaki wanaovuliwa kuwa ni kidogo.
1.4.3 BIASHARA
Baadhi ya wakazi waishio Lindi Mjini ni wafanyabiashara za jumla, rejareja na wafanyabiashara wadogo kama vile mama lishe.
1.4.4 VIWANDA
Viwanda ni moja ya shughuli za kiuchumi katika Mji wa Lindi japokuwa inafanywa na watu wachache sana wa Mji huu. Hii ni kwa sababu viwanda vingi vilivyokuwa vinafanya kazi katika miaka ya nyuma vimefungwa.

1.4.5 MADINI
Wilaya za Mkoa wa Lindi zina madini ya viwandani ambayo ni yenye tija kwa uwekezaji.
Mfano wa Madini ya viwandani yanayozalishwa mkoani ni pamoja na jasi katika Wilaya ya Kilwa, Ruangwa na maeneo ya Lindi Vijijini Jasi (Gypsum) hutumika kuzalisha sementi.
Madini ya vito yanayozalishwa na vikundi pia wachimbaji wadogo katika Wilaya ya Ruangwa, Nachingwea na Liwale pia katika maeneo ya Lindi Vijijini ni pamoja na Blue Supphire, Garnets, Tormaline, Aquamaline n.k.
Chumvi inazalishwa kwa utaratibu wa ukaushaji maji ya bahari kwa njia ya Solar Radiation. Wazalishaji wa Chumvi katika mwambao wa Wilaya za Kilwa na Lindi huzalisha chumvi kwa matumizi ya kiungio cha chakula na madini joto.


1.5 VYANZO VIKUU VYA MAPATO YA HALMASHAURI
Kama ilivyoelezwa hapo awali, kilimo ndio tegemeo kubwa la kipato cha wakazi wa Lindi Mjini kikifuatiwa na uvuvi kwani 50% hutegemea kilimo na 10% uvuvi. Hata hivyo pamoja na kilimo kuwa tegemeo kubwa la kipato cha wakazi wa Lindi Mjini, pato wanalolipata halijaweza kuisaidia sana Halmashauri yetu katika kuingizia mapato kutokana na uzalishaji mdogo wa mazao husika. Ili kuthibitisha hilo ni kwamba pato la wastani kwa mtu mmoja kwa Halmashauri hii ni Tshs. 223,191/= kwa mwaka ulioishia 2002. Hivyo kwa kifupi Halmashauri ya Mji wa Lindi inategemea zaidi mapato yake kutoka katika vyanzo vifuatavyo:
- Ada ya leseni za biashara.
- Kodi za majengo.
- Kodi ya ardhi.
- Ushuru wa mazao ya kilimo.
- Ushuru wa masoko.
- Ushuru wa mazao ya viwanda.
- Ushuru wa mazao ya biashara.
2.0 VYANZO VINGINE VYA MAPATO INAVYOTEGEMEWA NA HALMASHAURI YETU NI KUTOKA
2.1 SERIKALI KUU
• Mfuko wa Road Toll (Fedha ya barabaraba)
• Mfuko wa afya.
• Ruzuku ya mpango wa maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM)
• Ruzuku ya maendeleo (LGCDG).
• Ruzuku ya kujenga uwezo (CBG).
• Ruzuku ya mradi wa maji na usafi wa mazingira (RWSSP)
• Ruzuku ya mpango wa mazingira (UDEM).
• Ruzuku ya mpango wa sekta ya Kilimo (ASDP, DADP).
2.2 WAHISANI WENGINE
• Wa Kitaifa na Kimataifa.
• Ruzuku ya mradi wa kupambana na UKIMWI.
Pia wapo wafadhili wengine ambao wapo Halmashauri ya Mji wa Lindi kwa lengo la kusaidia kuondoa umaskini, wafadhili hawa wapo kwa lengo la kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kama vile mama lishe, mafundi seremala, mafundi cherehani n.k. Wafadhili hawa wapo chini ya UNDP pamoja na SIDO hata hivyo Serikali Kuu chini ya Wizara ya maendeleo ya jamii akina mama na watoto inatoa fedha kwa ajili ya kuwakopesha vijana na akina mama, pamoja na Halmashauri yenyewe kuchangia asilimia kumi (10) ya mapato yake kwa lengo hilo hilo la kutoa mikopo, ikiwa asilimia 5 ni kwa ajili ya akina mama na asilimia 5 kwa ajili ya vijana.
2.3 HUDUMA ZA JAMII
Huduma za jamii zinazoendeshwa hapa Halmashauri ya Mji wa Lindi zinahusisha Afya, Elimu, Maji na barabara, huduma hizi zinaendeshwa kutokana na fedha inayotolewa na Serikali Kuu, pamoja na makusanyo ya Halmashauri.
 
Top