Lindi Yetu Lindi Yetu Author
Title: TANROADS LINDI "YAKOMAA" NA MAGARI YANAYOZIDISHA UZITO, YAKUSANYA MILIONI 118
Author: Lindi Yetu
Rating 5 of 5 Des:
Na. Ahmad Mmow. Lindi WAKALA wa barabara(TANROADS) mkoani Lindi umefanikiwa kuiingizia serikali ...
Na. Ahmad Mmow. Lindi
WAKALA wa barabara(TANROADS) mkoani Lindi umefanikiwa kuiingizia serikali jumla ya shilingi 118,668,200/= kutokana na faini ya kosa la kuzidisha uzito kwenye magari.
Malori yakipima Uzito
Hayo yalielezwa na meneja wa wakala wa barabara wa mkoa wa Lindi, Issack Mwanawima, wakati wa kikao cha kawaida cha mkoa cha bodi ya barabara kilichofanyika jana katika manispaa ya Lindi.

Mwanawima alisema zoezi la kudhibiti uzito wa magari barabarani kwa kutumia mizani zilizopo Mingoyo na Nangurukuru katika kipindi cha kuanzia mwezi Machi hadi Oktoba mwaka huu, magari 153,681 yalipimwa.

Meneja huyo alisema katika kipindi hicho magari 1163 yalikutwa yamezidisha uzito kwa zaidi 5% inayoruhusiwa kisheria, hivyo zilitozwa kiasi hicho cha fedha ambacho hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu zilishalipwa.
"Takwimu zinaonesha kuna ongezeko kubwa la magari katika barabara ya Dar-eS-salaam, Lindi hadi Mtwara kutoka magari 75, 526 katika kipindi cha Agosti 2015 hadi Februari 2016 na kufia gari 153,681 kwa mwaka huu kuanzia kipindi cha mwezi Machi hadi Oktoba," alisema Mwanawima.

Mhandisi Mwanawima alisema upimaji wa kutumia mizani ndogo inayo hamishika uliohusisha magari yanayosafirisha saruji kutoka Mtwara kwenda Dar-es-Salaam, ulifanyika hivi karibuni yalikuwa na uzito wa kawaida. Hata hivyo upimaji uliofanyika katika maeneo ya Hotelitatu na Kiranjeranje, ulibaini kuwa hata yanayobeba mawe ya madini ya jasi(gypsum) yanayotoka migodini kwenda barabara kuu yalikutwa yamezidisha uzito takribani mara mbili ya unaotakiwa kisheria.

Aidha meneja huyo alibainisha kwamba katika mwaka wa fedha 2015/2016, mkoa huu ulitengewa shilingi 1.35 bilioni kutoka fedha za maendeleo kwa ajili ya kuzifanyia matengenezo barabara za mikoa zenye urefu wa kilometa 31.1.

Hata hivyo kutokana na upungufu wa fedha kwa mwaka wa fedha 2014/2015 kiasi hicho kilipunguzwa nakusababisha bajeti halisi kuwa shilingi 270.00milioni kwa mwaka wafedha wa 2015/2016.

Hata hivyo hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu hakuna fedha zilizopokelewa kwa miradi ya maendeleo. Mbali na hayo, mhandisi Mwanawima alisema jumla ya shilingi 1.00 bilioni zimetengwa kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Masasi, Nachingwea hadi Nanganga kwa kiwango cha lami. Ambapo nyaraka za zabuni zimeshawasilishwa makao makuu ya TANROADS katika mwaka wa fedha wa 2016/20017.

Kuhusu barabara ya Nanganga, Ruangwa, hadi Nachingwea. Meneja huyo alibainisha kuwa zimetengewa jumla ya shilingi 500.00 milioni kwa ajili ya kuanza upembuzi yakinifu na sanifu wa kina. Ambapo zabuni kwa ajili ya kumpata mhandisi mshauri ambazo tayari zimetangazwa, zimepangwa kurejeshwa tarehe 13 mwezi Desemba mwaka huu.
"Kazi za usanifu wa ujenzi wa daraja la Lukuledi zilikamilika mwezi Julai mwaka 2014,na kwa mwaka huu wa fedha kiasi cha shilingi milioni 51.00 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na zabuni kwa ajili ya kazi hiyo zimeshatangazwa," alisema Mwanawima.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi ambae alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho, aliwataka wakurugenzi watendaji wa halmashauri kufuatilia na kusimamia kwa karibu miradi ya ujenzi, ikiwamo ya barabara zinazojengwa na halmashauri zao.

Akibainisha wazi kwamba baadhi ya barabara na majengo ya umma yamejengwa chini ya viwango.

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

 
Top