Lindi Yetu Lindi Yetu Author
Title: AJABU YA "SITTA NA MUNGAI" MACHIFU WAWILI WANAOAGWA NDANI YA JUMA MOJA NA KUZIKWA KWENYE SIKU MOJA
Author: Lindi Yetu
Rating 5 of 5 Des:
Na. Maggid Mjengwa Ndugu zangu,  Samwel Sitta  ( 74) na Joseph Mungai ( 73) ni marafiki wa tangu...
Na. Maggid Mjengwa

Ndugu zangu, 
Samwel Sitta  ( 74) na Joseph Mungai ( 73) ni marafiki wa tangu Tabora Boys. Wawili hawa mama zao wanatoka kwenye koo kubwa za kichifu; Mama wa Samwel Sitta, Zuena Said Fundikira, ni binti wa Chifu Fundikira ambaye babu yake ni Mtemi Isike Kiyungi.
Samwel Sitta na Joseph Mungai
Mama wa Joseph Mungai  anatokana na ukoo wa Malangalila unatokana na Chifu Mkwawa.  Hivyo, akina Malangalila na Mwamuyinga ni wajomba zake Joseph Mungai kutoka  ukoo wa Kichifu wa Mkwawa.

Hivyo, wawili hawa mbali ya urafiki wao wa tangu shule uliowapelekea hadi kufanya kazi kama Mawaziri kwenye Serikali za Awamu Nne, pia ni watani wa jadi. Ni kwa vile Wahehe chini ya Chifu Mkwawa walipigana na  Wanyamwezi chini ya Mtemi Isike. 

Katika namna ya kusuluhisha mgogoro, Chifu Isike alimuozesha binti yake kwa Chifu Mkwawa. Kikosi kidogo cha Wakonongo kilitumwa na Isike kumsindikiza binti huyo. Walipoikaribia Iringa, Mkwawa alituma watu wake kwenda kumpokea binti huyo nje kidogo ya Iringa mahali ambapo hadi hii leo panaitwa Ikonongo.

Na Wakonongo wale waliamua kuweka makazi yao hapo. Ni nje kidogo ya Manispaa ya Iringa, na dalili za ujio wa Wakonongo hapo ni uwepo, hadi leo, wa watu wa asili ya Kikonongo na miti mingi ya miembe waliokuja nao Wakonongo kutoka Tabora, enzi hizo. 

Ni huzuni kwa vile marafiki hawa wawili hawakuweza kuagana. Na kwa vile, wote wawili  marafiki zao wengi ni wa wote wawili, basi, imebidi hata siku za kuwaaga Sitta na Mungai zipishane hata kwa siku moja ili marafiki wapate kuwaaga . 

Chifu Mungai ameagwa leo, na mwenzake Chifu Sitta ataagwa kesho. Wote wawili watazikwa katika siku moja ya Jumamosi, mmoja Mufindi  na mwingine Urambo.

Pumzikeni  Kwa Amani; Chifu Sitta na Chifu Mungai

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

 
Top