Lindi Yetu Lindi Yetu Author
Title: BENKI ZATAKIWA KUMALIZA MALALAMIKO YA WATEJA WAO
Author: Lindi Yetu
Rating 5 of 5 Des:
Na. Ahmad Mmow, Lindi. Katika kuhakikisha wateja wanaendelea kuhamasika kukopa, kuweka fedha na kuz...
Na. Ahmad Mmow, Lindi.
Katika kuhakikisha wateja wanaendelea kuhamasika kukopa, kuweka fedha na kuziamini benki zote nchini zimetakiwa kushughulikia na kumaliza malalamiko na migogoro mbalimbali dhidi ya wateja wake.

Ephraim Mwasunguti
Meneja Msaidizi dawati lakutatua malalamikoya wateja Benki kuu Ndg. Ganga Mlipano akiongea na Mwandishi wa Habari (Hayupo pichani) katika Viwanja vya Ngongo Lindi katiak maonesho ya Nane nane Kitaifa.

Wito huo ulitolewa jana na Meneja Msaidizi dawati lakutatua malalamikoya wateja Benki kuu Ndg. Ganga Mlipano, katika viwanja vya Ngongo manispaa ya Lindi yanapofanyika maonyesho ya nane nane kitaifa.

Mlipano alisema ingawa benki kuu imeunda dawati maalumu la kupokea, kusikiliza na kushughulikia malalamiko na migogoro ya wateja wa benki zote 57 zilizopo nchini, hata hivyo benki hizo zinawajibu wa kushughulikia na kumaliza malalamiko na migogoro dhidi ya wateja wake kabla ya kufikishwa benki kuu.

Alisema kushughulikia na kumaliza malalamiko ya wateja kutawajengea imani wananchi kwa benki hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi, ikiwa ni dhamira ya serikali. 


Akabainisha kwamba benki kuu imetengeneza mazingira wezeshi kwa wananchi wote, ikiwamo wakulima na wafugaji waweze kukopa ili kukuza vipato vyao na uchumi wa nchi ambapo benki hiyo imetoa leseni kwa makampuni ya karadha.

Pia meneja huyo alizitaka benki kutoa taarifa za wakopaji kwa benki hiyo kama mwongozo unavyoelekeza. Ambapo katika kuhakikisha taarifa za wakopaji zinafikishwa kwa wakati, benki kuu imesajili kampuni mbili ambazo kazi yake ni kukusanya taarifa za wakopaji wote, lengo likiwa ni kuwadhibiti wakopaji wasiotaka kulipa mikopo.

"Wadaiwa sugu ni miongoni mwa sababu za kufilisika benki, mpaka sasa benki tatu zimekufa na nyingine zilihuishwa baada ya kuwa na hali mbaya", alisema Mlipano.

Sanjari na hilo Mlipano alizikumbusha benki wajibu wa kuwatangazia wateja wake kwamba benki kuu inadawati maalumu la kupokea na kushughulikia malalamiko kuhusu jinsi benki kuu inavyohakikisha wananchi wenye vipato vya aina zote wanapata huduma za benki.

Alibainisha kuwa benki kuu imekuwa ikitoa leseni kuanzishwa benki nyingine ili kupanua wigo kwa wananchi kupata huduma na kuongeza ushindani katika utoaji huduma.

Akitolea mfano mwaka jana benki kuu ilitoa leseni kwa benki ya wakulima. "Kwa mfano kanda hii ya kusini, benki kuu imetoa leseni kwa benki ya wananchi ya Tandahimba, Jambo la msingi wananchi wajenge utamaduni wa kuweka, kukopa na kulipa kwa wakati kwa sababu wakopaji wasiolipa ndio wanaochangia benki kuwa na viwango vikubwa vya riba".

"Wakopaji wasiolipa wakidhibitiwa kunauwezekano viwango vya riba kushuka" aliongeza kusema Mlipano.

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

 
Top