Fungwa Kilozo Fungwa Kilozo Author
Title: #MAHABA:: KUJISIKIA NI SUMU MBAYA PENZINI, JIFUNZE..!
Author: Fungwa Kilozo
Rating 5 of 5 Des:
KWA wale ndugu zangu Waislamu, naamini tuko pamoja nanyi kiroho katika mfungo wa Mwezi Mtukufu wa R...
KWA wale ndugu zangu Waislamu, naamini tuko pamoja nanyi kiroho katika mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Swaumu najua inapanda na Mungu awafanyie wepesi, funga yenu iwe na swawabu na muimalize salama.
wapendanao kitandani
Baada ya salamu hizo, twende moja kwa moja katika mada yetu ya leo. Kama inavyojieleza hapo juu. Leo nazungumza na pande zote mbili ingawa tatizo au kasumba hii wanayo zaidi wanawake. Nitawazungumzia zaidi wanawake siku ya leo.

Ujana huwa una mambo mengi. Wakati ambao mwili unajengeka vizuri, unavutia, kuna hulka au kasumba huwa inaambatana na kipindi hicho, mtu kujisikia. Mwanamke huwa anajiona kwamba yeye ndiyo yeye.

Akili huwa inakuwa kama imezuzuka hivi. Ujana unamlevya. Haoni wala hasikii la mtu. Mawazo yake yote ni kuwa yeye ni bidhaa adimu. Akijitaza kwenye kioo, akisifiwa mtaani anajiona yeye ndiyo yeye. Hakuna kama yeye.

Anajifananisha na ua zuri lililochanua. Anajiona ni bidhaa adimu itakayoweza kuuzika wakati wowote. Kama vile nyuki wanavyotua katika ua zuri, anaamini na yeye ni ua zuri hivyo ni rahisi kila mwanaume kutaka kutua kwake.

Anaamini kutokana na umbo na sura nzuri aliyonayo, si rahisi kukosa mwanaume pindi inapotokea yule aliyenaye amemuacha. Anaamini leo atatua mwanaume huyu, ataondoka na kesho atatokea mwingine.

Kiburi cha ujana kinamuandama. Hakubali kuyumbishwa. Neno uvumilivu hataki hata kulisikia.

Hataki kuwa na mwanaume mwenye matatizo. Hataki kusikia neno shida. Anataka raha tu. Hahitaji karaha hata siku moja katika maisha yake. Akiona mwanaume analalamika kwamba mwezi fulani hajapata kitu kwa sababu biashara anayoifanya haikuwa nzuri, hataki kusikia kauli hiyo.

Anataka kuona anapewa fedha. Anataka kuona mwanaume anaingiza fedha za kutosha kuanzia Jumatatu hadi Jumapili, Januari hadi Desemba biashara iwe inaingiza faida tu. Kisiwepo kipindi cha kupata hasara.

Kisiwepo kipindi cha kupunguza fungu lake la matumizi kwa sababu ya kumtumia mama yake fedha za matibabu.

Anataka fedha za kumtibia mama zipatikane bila kuathiri fedha zake za saluni alizokuwa anapewa kila wiki. Hapendi kusikia ‘Kiswahili’ cha tofauti. Akipewa maelezo yatakayomfanya asipewe ‘mshiko’ wake wa kwenda kufanya ‘shopping’ ya nguo, haelewi.

Kwake shopping ina maana kuliko ugonjwa wa mama. Saluni ni bora kuliko fedha hiyo kuitumia kwa malipo ya ada ya mtoto ambayo mwezi huo imekosekana kutokana na biashara kuwa mbaya. Anaamua kujitoa penzini ili ampate mwanaume mwingine ambaye anaamini atampa kila kitu kwa wakati.

Anataka mwanaume ambaye atamsikiliza yeye na matakwa yake. Kama anataka fedha basi mwanaume asiwe na mkono wa birika. Atoe kila anapohitaji. Kama anataka kuheshimiwa basi mwanaume awe ananyeyekea. Asimpinge jambo lake.

Amuogope. Kila anachosema yeye ndicho sahihi. Anachokisema mwanaume siku zote ni batili. Mwanaume akikisimamia kile anachokiamini ni sahihi, hataki kumsikiliza. Yupo tayari kwa lolote. Hana cha kupoteza. Umri unamruhusu, atampata mwingine ndani ya muda mfupi tu.

Ili kumdhihirishia kwamba yeye ni bidhaa adimu, mwanamke anahakikisha anapata mbadala fasta. Tena si tu anapata mbadala bali anahitaji kumuonesha yule mwanaume wake wa awali kwamba yeye bado analipa. Anauzika.

Anajitahidi kumuonesha kwamba umri bado unaruhusu. Moyoni anajisemea; “mimi kifaa bwana.” Anaamini kwamba hata huyo mpya anaweza kummwaga na akapata tena mwingine na mwingine pasipo kuwa na kikwazo chochote.

CHUKUA HII KUTOKA KWANGU

Maisha tuliyonayo ni mafupi. Huna sababu ya kuufanya mwili wako majaribio, leo utakuwa na huyu kesho yule. Wengi sana wamejikuta kwenye majuto kwa kuendekeza staili hiyo. Kuishi kwa kubadilibadili uhusiano siyo sifa. Kunakupotezea muda. Tengeneza maisha na uliye naye.

Kuwa mvumilivu. Hakuna maisha rahisi. Kuna kupanda na kushuka, kuna shida na raha. Kila aliyefanikiwa kwenye uhusiano ana historia yake. Itengeneze ya kwako angali ukiwa na umri mdogo. Tulia.

Ukipata uhusiano unaouna ni sahihi, shikilia hapo katika shida na raha na mwisho wa siku Mungu ataweka baraka zake mtafika mbali. Kilele chenu kitakuwa na mafanikio!

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

 
Top