Fungwa Kilozo Fungwa Kilozo Author
Title: MKUU WA WILAYA, MKURUGENZI SHINYANGA WAMKANA ANNA KILANGO
Author: Fungwa Kilozo
Rating 5 of 5 Des:
Siku moja baada ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango kuvuliwa uongozi kwa kutosema...
Siku moja baada ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango kuvuliwa uongozi kwa kutosema ukweli, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani humo, Hawa Ng’humbi ameiruka taarifa ya kutokuwapo kwa watumishi hewa, ambayo amesema ilimshtua alipoiona kwenye televisheni.
Hawa Ng’humbi

Rais John Magufuli juzi alitengua uteuzi wa Kilango, ikiwa ni siku 30 tangu alipotangaza kumteua kwa maelezo kuwa alitoa taarifa isiyo ya kweli kuwa Shinyanga hakuna watumishi hewa kabla ya kujiridhisha.

Pamoja na Kilango, Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Katibu Tawala wa Shinyanga, Abdul Dachi, kwa sababu hiyo ya kutoa taarifa za uongo.

Dk Magufuli alichukua uamuzi huo baada ya kutuma timu mkoani Shinyanga kufanya uhakiki na kubaini kuwa kulikuwa na watumishi hewa 45 katika wilaya moja ya Shinyanga kabla ya kwenda wilaya nyingine za Kahama na Kishapu.

Akizungumzia sakata hilo jana baada ya uamuzi wa Dk Magufuli, Ng’humbi alisema taarifa za kukosekana watumishi hewa kwenye wilaya yake alizisikia kwenye taarifa ya habari ya televisheni Machi 30 na zilimshtua. “Binafsi nilishtuka sana nilipoona ikitangazwa kuwa mkoa mzima wa Shinyanga, hakuna mfanyakazi hewa wakati mimi sikuwa hata nimeona taarifa kutoka wilayani kwangu iliyoandaliwa na uongozi wa halmashauri, Nilijiuliza taarifa imefikaje kwa mkuu wa mkoa bila kupitia kwangu? Kusema kweli nilianza kuifanyia kazi taarifa hiyo na ninatarajia ifikapo Ijumaa nitakamilisha kazi hiyo.” alisema Ng’humbi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Alphonce Gagambobyaki alisema hadi sasa ofisi yake haijafahamu nani aliyempa mkuu wa mkoa taarifa ya ukaguzi wa wafanyakazi hewa kwa sababu taarifa aliyonayo mezani haijasainiwa. “Kuna tatizo la ofisi hii kukaimiwa na zaidi ya watu wanne tangu aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji, Dalikunda Kimulika alipostaafu Februari. Ni vigumu kujua nani alihusika nayo bila kuona saini, alisema Bagambobyaki, Wakati bado tunajiridhisha kujua ni ruhusa ya aina gani na hawa watumishi wako wapi, ndipo taarifa ilipotangazwa kwamba mkoa hauna watumishi hewa,” alisema.

Kilango ambaye juzi alisema hakuwa amepata taarifa hivyo asingeweza kuzungumzia kutenguliwa kwake, jana alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kabisa na Dachi akaeleza kuwa ameupokea uamuzi huo kwa kuwa Rais ndiye mteule wake.

Credit: Mwananchi

About Author

Advertisement

 
Top